'Cannavaro' amesema imewauma sana kupoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC na kushindwa kutetea taji lao.

Nahodha wa Yanga Nadir Horoub 'Cannavaro' amesema imewauma sana kupoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC na kushindwa kutetea taji lao.

Cannavaro ameiambia Goal, hawakuyategemea matokeo hayo kutokana na ubora wa kikosi walichonacho ukilinganisha na kile cha Mbao FC.

"Leo nimeamini kwenye soka kuna bahati tumecheza muda wote langoni mwao lakini tulikosa bahati ya kuzitumia nafasi tulizopata nikiwemo mimi mwenyewe," amesema Cannavaro.

Nahodha huyo amewapongeza Mbao FC kwa kucheza kwa nidhamu muda wote wa mchezo na kufanikiwa kulinda bao lao la dakika ya 26 ambalo mchezaji wa Yanga Andrew Vicent alijifunga katika harakati za kuokoa.

Cannavaro amesema anatambua matokeo hayo yamewaumiza sana mashabiki wao lakini watajipanfa kuhakikisha wanarudisha furaha yao kwa kutwaa ubingwa wa ligi ya Vodacom.

"Tunawaomba radhi mashabiki wetu nasema tulikosa bahati kwasababu tulishambulia sana lakini tulishindwa kuzitumia nafasi tulizozioata tumekubali matokeo na tuna watakia kila la kheri katika mchezo wao wa nusu fainali," amesema.

Yanga inatarajiwa kurejea Dar es salaam leo ikijiandaa na mchezo wa ligi ya Vosacom dhidi ya Kagera Sugar ambao utapigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Mei 6.