Wengi wamekuwa wakiandika ujumbe kuwaliwaza Yanga ambao msiba unawahusu kwa kuwa ni shabiki wao, msiba huo wa Ally Yanga ni wa taifa na wapenda soka

Mabingwa wa soka Ligi Kuu Tanzania bara kwa mara tatu mfululizo klabu ya Yanga wamepatwa na msiba mzito baada ya moja ya aliyekuwa mshabiki wao maarufu kama Ally Yanga kufariki kwa ajali ya gari.

Ally Yanga kama anavyofahamika amefariki hii leo mchana jijini Dodoma ambako taarifa zinasema alikuwa kwenye shughuli za kukimbiza mwenge.

Yanga alikuwa maarufu sana katika ushangiliaji kutokana na aina yake ya kipekee ya kujipaka mkaa usoni na kujaza nguo katika tumbo lake kama ana kitambi.

Kutokana na msiba huo aliyekuwa msemaji wa klabu ya Simba bwana Haji Manara ametuma salamu za pole kwa watani wake hao na akisema amehuzunishwa na msiba huo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika “nimepigiwa simu kwamba Ally Yanga amefariki huko Mpwapwa mkoani Dodoma, msiba huu ni wetu wote na tunawapa pole watani zetu.”

Goal inatoa pole na inaungana na wadau wote wa soka Tanzania kuomboleza msiba wa shabiki huyo aliyefariki dunia.