Simba imezidi kuwatia presha mabingwa watetezi wa ligi ya Vodacom Yanga baada ya leo kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United

Simba imezidi kuwatia presha mabingwa watetezi wa ligi ya Vodacom Yanga baada ya leo kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United katika pambano lililopigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Ushindi huo umeirudisha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 65 na kuwashusha Yanga katika nafasi ya pili wakibakiwa na pointi zao 62 na michezo mitatu mkononi huku Simba ikiwa imesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Mwadui FC.
Selemani Khassim alikuwa wa kwanza kuwaweka wageni mbele baada ya kuifungia Stand United bao la kuongoza sekunde ya tano ya mchezo baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa nahodha Jakob Massawe na kuweka hofu kwa mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakitamani timu yao kuibuka na pointi tatu katika mechi hiyo.
Baada ya kufungwa bao hilo Simba ilicharuka na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Stand United lakini mshambuliaji Laudit Mavugo na Shiiza Kichuya walishindwa kuzitumia nafasi nyingi walizopata.
Mshambuliaji Juma Luzio aliisawazishia Simba bao dakika 23 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Shiiza Kichuya ambapo mpira ulimshinda kipa wa Stand United Hamza Mwonge na kujaa wavuni.
Bao hilo liliwapa hamasa wachezaji wa Simba na kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Stand United na dakika ya 35 Luizio tena aliifungia Simba bao la pili baada ya kumalizia mpira ambao mabeki wa Stand walishindwa kuundoa kwenye eneo la hatari.
Wachezaji wa Stand walilalamikia bao hilo wakidai Luizio alikuwa ameotea lakini mwamuzi Imani Mwandembwa aliendelea na msimamo wake kwa kulikubali bao hilo ambapo matokeo hayo yalidumu mpaka mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Stand lakini umaliziaji ulikuwa mbovu huku kipa Hamza Mwonge akiokoa baadhi ya michomo hatari langoni mwake.
Stand United walikuja juu na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Simba lakini mshambuliaji wake Kheri Khalifa alishindwa kuitumia nafasi ya kuisawazishia timu yake dakika 61 wakati alipopokea pasi nzuri ya Frank Khamisi.
Simba walifanya mabadiliko dakika ya 62 kwa kumtoa Mohamed Ibrahim na kumuingiza Mwinyi Kazimoto mabadiliko ambayo hayakuonyesha matunda kwa upande wa Simba zaidi ya kuwapa nafasi Stand kuutawala mchezo.
ဆင်ဘာ
Stand United
မှတ်ချက် အားလုံး (1)
8-26 22:41