Banda amesema anaondoka kwenye klabu hiyo akiwa anajivunia kombe la FA alilowaachia mashabiki wa timu hiyo

Beki wa klabu ya Simba Abdi Banda amesema anaondoka kwenye klabu hiyo akiwa anajivunia kombe la FA, alilowaachia mashabiki wa timu hiyo aliyoichezea kwa mafanikio makubwa.

Banda ameiambia Goal, anakwenda kucheza soka Afrika Kusini, na mipango yake inakwenda vizuri baada ya kusaini mkataba wa awali na moja ya timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza.

"Huu ni mpango uliokuwepo kwa muda mrefu na nilishakwenda kusaini mkataba wa awali na kilichobaki ilikuwa ni kumaliza msimu na mkataba wangu hapa Simba,"amesema Banda.

Beki huyo amesema atawamissi sana wachezaji wenzake pamoja na sapoti kubwa ya mashabiki wa timu hiyo lakini amesema siku zote ataendelea kuwakumbuka kutokana na ushirikiano mkubwa waliompa.

Amesema mafanikio aliyokuwa nayo yametokana na Simba hivyo siku zote ataiheshimu klabu hiyo kwani imetimiza ndoto zake za kucheza soka nje ya nchi.

"Ilikuwa ni ndoto zangu za muda mrefu siku moja kucheza soka nje ya Tanzania nafurahi kuona zinaelekea kukamilika kwani msimu ujao sitovaa tena jezi ya Simba wala ya timu yoyote hapa Tanzania,"amesema Banda.

Mechi ya Kombe la FA, ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa Banda ambaye alidumu kwa misimu miwili akitokea Coastal Union ya Tanga